Je, Dawa ya kukoroma ni nini?
Swali hilo limeulizwa sana na mimi katika kulijibu ningependa kusema kuwa, kujua sababu inayosababisha mtu akorome na kuitatua au kuiondoa sababu hiyo ndiko kunakotibu kukoroma. Sote tunajua adha inayotokana na kukoroma, na sauti hiyo inavyosumbua hasa iwapo anayekoroma ni mtu wako wa karibu kama vile mumeo, mwenzi wako au yoyote yule inayekubidi ulale naye karibu au katika kitanda kimojana hata chumba kimoja. Kukoroma pia huathiri usingizi wa mkoromaji kwani anayekoroma humbidi aamke mara kadhaa usingizini akijua au bila kujua kutokana njia zake za hewa kufunga kwa sekunde kadhaa ambapo usingizi pia hukatika. Wanaokoroma pia hushindwa kulala vizuri suala linalopelekea asubuhi wawe wamechoka na kutofanya majukumu yao vyema, na pia wale wanaolala nao karibu hupatwa na matatizo kama hayo. Vilevile tunapaswa kujua kuwa kukoroma kuna athari za kiafya za muda mrefu kwa mtu anayekoroma hivyo si jambo la kufanyia mzaha na ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa. Wataalamu wanatuambia kuwa ili kujua kukoroma kwako kunasababishwa na nini ni bora ushirikiane na mwenzi wako au yoyote unayelala naye ili akuchunguze pale unapolala na kujua jinsi mwili wako unavyokuwa pale unapokoroma.Ni bora aandae orodha na kuchunguza yafuatayo:
1. Kufunga mdomo na kukoroma kunaonyesha kuwa kuna matatizo ya ulimi. 2. Kufungua mdomo na kukoroma kunaonyesha unaweza kuwa na tatizo katika misuli au nyama za koo. 3. Kukoroma unapolala kichalichali kunaonyesha kuwa pengine kwa kubadilisha namna unavyolala kukoroma nako kunaweza kwisha. 4. Kukoroma wakati unapolala kwa kila mlalo kunaonyesha kwamba tatizo lako ni kubwa na pengine kunahitajia tiba kubwa zaidi.Tiba
Iwapo umebadilisha namna unavyolala na haikusaidia, unashauriwa ujaribu yafuatayo:Punguza uzito
Safisha njia yako ya hewa.
Kuwa na pua iliyoziba hufanya kupumua kuwe kugumu na kusababisha kukoroma. Unaweza kufanya hivyo kwa kutumia dawa za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana kwa urahisi katika maduka ya dawa.Wacha kuvuta sigara.
Lala mapema na pata usingizi wa kutosha kila mara huku ukijiepusha na kuchoka sana.
Nyanyua kichwa
Kunyanyua kichwa kwa nchi 4 huweza kupunguza kasi ya kupumua na kusaidia ulimi na taya kwenda mbele hali ambayo hupunguza kukoroma. Fanya hilo kwa tumia mito maalum ya kupunguza kukoroma au lala bila mto.Kula vyakula hivi
Wataalamu pia wanasema kwamba unaweza kupunguza kukoroma kwa kutokula baadhi ya vyakula au dawa kabla ya kulala ambavyo huongeza kukoroma. Vitu hivyo ni kama vile;- Kutokula mlo mkubwa kabla ya kulala.
- Kutokula vyakula vinavyotokana na maziwa au maziwa ya soya.
- Kutokunywa pombe kabla ya kulala.
- Kutotumia dawa aina ya antihistamines.
- Kutotumia vyakula au vinjwaji venye kafeini.